Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya mashindano wakati Young Africans iliposhiriki kwa mara ya mwisho hatua ya Makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Hussein Nyika amedai kuwa wanaicheka Simba kutolewa kiutani, lakini kuna kitu wanajifunza.
Simba SC ilishindwa kusonge mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, licha ya kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Kaizer Chiefs, Jumamosi Mei 22, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mabao manne kwa sifuri waliyofungwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa Afrika kusini Mei 15, ndio yamewasukuma nje ya michuano hiyo Simba SC.
Kutokana na hali hiyo Nyika amesema suala la kuwacheza Simba SC, ni kawaida kutokana na utani uliojengeka baina ya timu hizo, lakini ukweli ni kwamba kuna mengi yanapaswa kuchukuliwa kama funzo kwa upande wa Young Africans ambao huenda wakashiriki michuano ya Afrika msimu ujao.
Nyika amesema: “Nimeangalia mtani (Simba) hajapoteza nyumbani msimu huu, hii ni rekodi bora sana kwao inayowafanya kulinda hadhi yao. Nilichogundua Simba ni wamoja, hawabaguani inapokuja suala la kulinda heshima ya klabu yao.
“Hapa lazima Yanga wenzangu tujifunze kupitia hili hata kama kafanya Simba, hata wao walijifunza kutoka kwetu katika kutulia na kusajili timu tishio wakiachana na kutumia wachezaji watoto.
“Ukiangalia mashabiki wa Simba na viongozi wao walikuwa sambamba na wachezaji wao na kuwasaidia kupata mabao yale matatu, Kilichonivutia ni mwisho wa mchezo wote waliwapongeza wachezaji wao, hali ile inamjenga mchezaji kujiona ana thamani ya kuzidi kuipigania timu yake.
“Usajili ni kamari, sawa kuna maeneo unaweza kufanikiwa na usifanikiwe lakini tunatakiwa kuwa makini halitakiwi hili la kusajili kuwa la watu wawili watatu pia wanatakiwa kuwa na fikra za kuangalia jinsi eneo hili lilivyotukwamisha msimu huu.”