Mwanasheria wa Klabu ya Young Africans Simon Patrick ameungana na baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Klabu hiyo kuonyesha hisia za kushindwa kuibuka na ushindi dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Young Africans jana Jumatano (Novemba 02), ilicheza mchezo wa Mkondo wa Kwanza hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho Barani Afrika nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam na kuambulia sare ya bila kufungana.
Mwanasheria Simon Patrick ameonesha hisia za kushindwa kufanya vizuri kwenye mchezo huo kwa kuandika ujumbe mzito katika Ukurasa wake za Mitandao ya Kijamii wa Instagram, akikubaliana na kinachoendela kwa Mashabiki na Wanachama.
“Wanachokifanya mashabiki wa Yanga kutoa ya moyoni ni sahihi kabisa kwani ndiyo haki kubwa waliyonayo.
Kama Viongozi tumeumizwa sana na matokeo ya jana ukizingatia tumefanya kila kitu kiutendaji kwa ajili ya kuwafurahisha mashabiki wetu lakini mambo hayakwenda kama tulivyotarajia.
Uongozi huu ni sikivu sana, umepokea na unaendelea kupokea maoni na ushauri wenu, tutayachakata na kuyafanyia kazi.
Rais wetu na Kamati ya Utendaji wamejitahidi kuhakikisha Yanga ina kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya timu, lakini matokeo yamekua kinyume na matarajio.
Nawaomba tuendelee kuisapoti timu yetu kwenye mchezo wa marudiano Tunisia, mambo mengine tuwaachie viongozi mliowapa dhamana, wana malengo makubwa sana na timu,”