Chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe, MDC kimetangaza kuahirisha mpango wake wa kutaka kumuapisha aliyekuwa mgombea wake wa urais, Nelson Chamisa kama ‘Rais wa Wananchi’, wakifuata nyayo za Raila Odinga wa Kenya.
Uamuzi huo wa MDC umewekwa wazi kufuatia tangazo la Serikali la kupiga marufuku mikusanyiko kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.
MDC ilidai kuwa mpango wake wa kumuapisha Chamisa ulilenga kutoa ujumbe kuhusu kile wanachodai ni kuchakachuliwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais wa Julai 30 mwaka huu, wakidai kuwa mgombea wao ndiye aliyeshinda na sio Rais Emmerson Mnangagwa aliyetangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Chama hicho kimeilalamikia Serikali kwa madai kuwa imetumia ugonjwa wa kipindupindu kama sababu ya kuzuia mkutano wao, kinyume cha uhalisia.
“Iko wazi kuwa Serikali imetumia vibaya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa malengo ya kisiasa na inatupa shaka kuwa tangazo lao limelenga kuharibu mkutano wetu,” alisema msemaji wa MDC, Jacob Mafume.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Afya nchini humo, ugonjwa wa kipindupindu umesababisha vifo vya watu 25 jijini Harare.
Mahakama Kuu nchini humo ilibariki ushindi wa Rais Mnangagwa katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi iliyofunguliwa na Chamisa.
Hatua ya MDC kutaka kumuapisha Chamisa inafanana na ile ya muungano wa chama kikuu cha upinzani nchini Kenya kumuapisha Raila Odinga kama ‘Rais wa Wananchi’, wakipinga matokeo ya uchaguzi uliompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta.