Wizara ya afya nchini Burundi, ilmeangaza kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu katika jiji la Bujumbura, ambapo wagonjwa zaidi ya 10 wameripotiwa kulazwa Hospitalini.
Waziri wa afya wa nchi hiyo, Sylvie Nzeyimana amesema sampuli ambazo zilichukuliwa kwa uchunguzi na majibu kutolewa Jumamosi iliyopita, zimeonyesha kuwepo kwa viini vinavyosababisha kipindupindu.
Amesema, maambukizi yameripotiwa pia katika maeneo ya Bukirasazi, Mutakura ikiwa yanatukia kipindi ambacho mji wa Bujumbura na viunga vyake ukikabiliwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Hata hivyo, amesema tayari serikali imechukua hatua kudhibiti mlipuko huo ikiwemo kunyunyiza dawa katika makazi ya watu, kuhamasisha jamii na kuwatafuta watu walioathirika, huku shirika la madaktari wasio na mipaka MSF, likisema ugonjwa huo huathiri kati ya watu 200 – 250 kila mwaka nchini Burundi.