Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe amenyang’anywa Ofisi yake ya Ubunge na Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na kuagiza itumiwe na Idara ya Uhamiaji.
Ole Sabaya amefikia uamuzi huo kwa kile alichodai kuwa ameelezwa kuwa Mbowe hajaitumia ofisi hiyo tangu mwaka 2010, hivyo haina haja kuendelea kuwepo na kutotumika katika matumizi yaliyo kusudiwa.
“Tangu Mbowe achaguliwe Mwaka 2010 hajawahi kuingia katika Ofisi hiyo kusikiliza kero za wananchi, sijui yupo wapi namsikia huko maeneo mengine akifanya vurugu, sasa ofisi hii itatumika kusaidia wananchi”, amesema Ole Sabaya.
Mbowe amenyang’anywa ofisi hiyo akiwa gerezani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwafutia dhamana Novemba 23, 2018 kwa kukiuka masharti ya dhamana ikiwemo kutoka nje ya nchi bila kibali, yeye pamoja na Mbunge wa Tarime Mjini Ester Matiko.
Mbowe na Matiko wako mahabusu baada ya kufutiwa dhamana kwenye kesi yao ya msingi inayowakabili juu ya kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa NIT, Akwilina Akwilini baada ya kufanya maandamano kuelekea katika ofisi za Mkurugenzi wa Kinondoni Februari 2018.