Aliyekuwa kocha wa klabu ya Simba Jamhuri Kiwelu Julio amemtaka kiungo wa mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC Ibrahim Ajib, kuacha tabia ya kucheza mpira kwa kujifurahisha na acheze mpira kama kazi.
Julio amemtaka kiungo huyo kubadilika, baada ya kumfuatilia kwenye mchezo wa jana dhidi ya Ruvu Shooting, uliomalizika kwa Simba SC kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.
Julio ambaye alikua sehemu ya wafuatiliaji wa mchezo huo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, amesema anampenda sana mchezaji huyo kuliko wachezaji wengine wote Tanzania, na ndio maana amechukua jukumu la kumkumbusha wajibu wake wa kucheza mpira kama kazi, na sio kujifurahisha mwenyewe.
“Mie nampenda sana Ajib kuliko mchezaji yoyote Tanzania isipokuwa yeye anacheza kama yupo yupo tu hajitumi hachezi mpira kama kazi, anacheza kwa kujifurahisha tu, lakini kama atabadilika na kucheza mpira kama kazi Ajibu ni mchezaji mzuri sana.” amesema Julio.
Kwa mara ya kwanza msimu huu, Ajib alipata nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha Simba, lakini hakuonesha umahiri wowote wa kuisaidia timu yake kupata matokeo chanya.