Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Selemani Jafo amesema Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani imetekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali ya kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa mwaka.
Jafo ameyasema hayo wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 wilayani humo wenye kaulimbiu ‘Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa’ Amesema katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa na kutunzwa halmashauri ya wilaya hiyo imevuka lengo la kupanda idadi hiyo ya miti.
“Hatuigizi bali tunafanya kwa vitendo sisi tumezidisha malengo ya upandaji miti kwa mwaka na tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kuhusu utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji,” amesisitiza Dkt. Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe.
Akiendelea kuzungumza wakati wa ukaguzi wa miradi ya Mwenge wilayani humo amesema ‘Kampeni ya Soma na Mti’ imeendelea kushika kasi na linatekelezeka kwani kila mwanafunzi kutoka shule mbalimbali anapanda mti.
Aidha, Waziri Jafo ameelezea kuhusu namna Msitu wa hifadhi wa Pugu Kazimzumbwi uliopo wilayani humo na kusema umeleta faida kubwa zikiwemo utalii wa ndani na hivyo kuingiza mapato.
Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokea nchini na duniani kwa maeneo mbalimbali Serikali na washirika wa maendeleo imekuwa ikipeleka miradi kwa ajili ya kukabiliana changamoto hiyo hivyo Mwenge wa Uhuru pia umetembelea Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi wilayani humo.