Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya, KEMRI imesema imegundua aina mpya ya ugonjwa wa kisonono, unaosambaa kwa kasi katika jiji la Nairobi, hasa kwa watu wanaojihusisha na biashara ya ngono jinsia ya Ke.
KEMRI imesema, ongezeko hilo limetokana na taarifa potofu kuwa baadhi ya makahaba ambao wanaotumia dawa za kujikinga na maambukizi ya VVU, kuamini kuwa dawa hizo zitawaepusha na magonjwa ya zinaa hivyo kushiriki ngono bila kinga.
Majibu ya utafiti juu ya ugonjwa huo, yametokana na ushirikiano wa makahaba zaidi ya 350 waliofika Zahanati moja ya jijini Nairobi, ambayo iliripoti visa vingi vya ugonjwa wa kisonono huku robo tatu ya waliohojiwa, wakikiri kufanya mapenzi bila kinga.
Hata hivyo, baadhi yao walikiri kulala na angalau wateja 29 kwa kipindi cha wiki mbili na sasa KEMRI inaitaka Serikali ya Kenya kubadilisha sera ya sasa ya matibabu pamoja na kuhimiza raia kupima afya zao.