Baba mzazi wa Nahodha na Mshambuliaji wa FC Barcelona Lionel Messi, bado yupo kwenye mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo, kufuatia sakata la mwanaye kuhitaji kuondoka katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya wa soka barani Ulaya.
Jorge Messi ambaye pia ni wakala wa Messi, aliwasili mjini Barcelona jana Jumatano na kuanza mazungumzo na viongozi, ili kuweka mambo sawa ambayo yataamua mustakabali wa mwanaye, ambaye anahusishwa na mpango wa kutaka kufanya kazi na meneja wake wa zamani Pep Guardiola anaekinoa kikosi cha Manchester City.
Inaelezwa kuwa Jorge alienda kufanya kikao na Rais wa Barca Josep Bartomeu akiwa ametokea England ambapo ripoti zinadai kuwa alienda kukutana na viongozi wa Manchester City ili kufanya uhamisho wa mchezaji wake.
Mpaka sasa ndani ya Barca inaelezwa kuna mvutano kwa viongozi wenyewe kwa wenyewe, kuna baadhi wanaamini ni vizuri Messi auzwe ili kupunguza gharama za uendeshaji wa timu kwa kuwa mshahara wake uliobakia ni zaidi ya Euro milioni 100, hivyo akiuzwa klabu itaepukana na gharama hiyo. Lakini kuna wengine wanapinga hilo.
Messi ambaye ana umri wa miaka 33, juma lililopita mwana sheria wake aliwasilisha maombi kwa Barca kuwa mteja wake anahitaji kutumia kipengele kilichopo kwenye mkataba wake ambacho kinamfanya kuwa mchezaji huru kabla ya msimu wa 2020-21 kuanza, ili kuondoka klabuni hapo.
Lakini suala hilo llipanguliwa na Barca ambao walieleza kuwa kipengele hicho kilikufa tokea Juni, 10, huku wakati huo huo kuna taarifa zinazodai kuwa tayari baba yake huyo amemalizana na mabosi wa City na amekubaliana nao kuwa Messi atasaini mkataba wa miaka mitano huku Pauni 600 milioni ikitarajiwa kutolewa.
Mwamba huyo ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2021, hatma yake inatarajiwa kujulikana leo baada ya kikao hicho.