Klabu ya Kitayosce (Tabora United) imeanza vita vya kushusha watu kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ambapo imebakiza hatua chache kumalizana na kocha Mserbia Goran Kopunovic.
Timu hiyo ambayo itashiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu baada ya kupanda msimu uliomalizika imekamilisha hatua kubwa ya mazungumzo na kocha huyo wa zamani wa Simba SC.
Kocha huyo anaweza kutua nchini leo kumalizia hatua za mwisho za kusaini mkataba wa mwaka mmoja na timu hiyo yenye makazi yake mjini Tabora.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo ni kwamba, baada ya kumalizana na Goran matajiri wa Kitayosce (Tabora United) wataanza kushusha mastaa wapya kwa ajili ya msimu ujao.
Bosi mmoja amesema kuwa Goran baada ya kusaini mkataba atapewa nafasi ya kuwapitisha mastaa wapya wa kigeni wanaotarajiwa kusainishwa mikataba.
“Kocha atawaangalia ndio maana mnaona amekuja mapema. Sisi sio watu wa kupokonyana wachezaji. Sisi wenyewe soko la watu bora tunajua kuwapata,” amesema.
“Tutaleta watu tofauti na hawa ambao mmekuwa mkiona wanatajwa kwamba tutawasajili, lakini kocha atakuwa wa mwisho kubariki kama nani tumpe mkataba na nani tusimpe.”