Naibu Kiongozi wa chama cha CDU ambaye ni Waziri wa Afya Jahn Spahn akizungumza na kituo cha redio cha taifa cha DeutschlandFunk, amesema vyama vya kisiasa vinapaswa kufikia mwafaka katikati ya mwezi Oktoba kuhusu nani watakaoshiriki kwenye mazungumzo rasmi ya kuunda serikali ya mseto, ili kila mmoja afahamu nchi inaelekea wapi.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na mgombea aliyewania kumrithi kutoka kambi yake ya wahafidhina, Armin Laschet wamempongeza mgombea wa ukansela wa chama cha Social Democratic, SPD Olaf Scholz kwa kushinda uchaguzi uliofanyika siku ya Jumapili.
Laschet alikuwa akikosolewa sana kwa kushindwa kumpongeza mapema mpinzani wake huyo aliyeshinda uchaguzi wa Jumapili.
Huku Juhudi za kutafuta maelewano ya kuunda serikali zaendelea wakati miito ikitolewa kuwataka wanasiasa wajitahidi kutoa msimamo katikati ya mwezi Oktoba.
Hivi sasa Scholz ambaye ni waziri wa fedha katika serikali ya mseto ya Kansela Merkel anatafuta namna ya kufikia makubaliano na chama cha Kijani kilichopata asilimia 14.8 ya kura pamoja na Free Democratic FDP kilichopata asilimia 11.5 ya kuunda serikali mpya alau kufikia Krismasi na anasema amekabidhiwa mamlaka na wapiga kura kuunda serikali ikiwezekana.