Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imewafungia maisha wanafamilia wawili kujishughulisha na mpira wa miguu, baada ya kuwakuta na hatia ya Upangaji Matokeo.
Taarifa iliyotolewa na TFF mapema leo Ijumaa (Mei 12) asubihi, imeeleza Mwenyekiti wa Kitayosce FC Yusuph Kitumbo na Kocha Ulimboka Mwakingwe ndio wahusika katika sakata hilo, ambalo linapigwa vita michezoni.
Wawili hao wametiwa hatiani baada ya kujihusisha na upangaji matokeo katika mechi ya Ligi ya Championship kati ya Fountain Gate FC na Kitayosce FC iliyochezwa Aprili 29 mwaka huu mjini Gairo, Morogoro.
Kamati ya Maadili katika kikao chake kilichofanyika jana Alhamis (Mei 11) mwaka huu imewatia hatiani wawili hao kwa kuzingatia Ibara ya 73(9) (b) ya Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la 2021.
Hata hivyo Kitumbo hakufika mbele ya Kamati bila kutoa udhuru wowote wa maandishi ya kupokea wito, wakati Mwakingwe aliwasilisha utetezi wake kwa njia ya maandishi.
Uamuzi kamili utatolewa kwa maandishi kwa pande husika katika mashauri hayo mawili.