Klabu ya Simba SC huenda ikafanya usajili mwingine wa Mchezaji wa Kimataifa, endapo itashawishika kumuuza Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal, Pape Ousmane Sakho.
Simba SC inatajwa kuwa kwenye mpango wa kushawishika na ofa ya Mabingwa wa Soka Barani Afrika Wydad Casablanca, ambao wameonyesha kuvutiwa na uwezo wa Sakho, hasa baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa Bao Bora la CAF 2022.
Klabu hiyo ya nchini Morocco imejipanga kumng’oa Sakho Msimbazi kwa dili la Shilingi za Kitanzania 1.6.
Endapo Simba SC itaingia kwenye Biashara ya kumuuza Sakho, inatajwa huenda ikaangukia kwa Kiungo Mshambuliaji mwingine kutoka Ivory Coast anayekipiga kwenye klabu ya Ismailia ya Misri Jean Morel Poé.
Poé anayemudu vizuri kucheza winga zote kama ilivyo kwa Sakho, lakini ameongezewa uwezo pia wa kucheza kiungo mshambuliaji wa kati na Mshambuliaji wa mwisho kwa maana ya namba tisa.
Chanzo cha uhakika kutoka katika Kambi ya Simba iliyopo Mji wa Ismailia nchini Misri, kimesema kwamba uongozi wa klabu hiyo upo kwenye majadiliano mazito juu ya kumsajili mwamba huyo anayewachezea Waarabu wa Misri, timu ya Ismailia.
Mtoa taarifa huyo ambaye wakati anazungumza alikuwa akijiamini sana, amesema Kocha Zoran Maki ndiye amependekeza Poé asajiliwe baada ya kumuona wakati wa mechi ya kirafiki walioyocheza dhidi ya Ismailia na kutoka sare ya bao 1-1.
“Huyu jamaa siyo straika moja kwa moja, ni mtu wa pembeni, tulicheza naye mechi ya kirafiki ile dhidi ya Ismailia tuliyotoka sare ya 1-1.
“Ni mchezaji mzuri sana, watu walivutiwa naye, ukiangalia kikosini kwetu kwa sasa tuna wachezaji wa pembeni wengi, lakini uongozi unaangalia namna ya kumsajili kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zote za mbele ikiwemo mshambuliaji wa mwisho.
“Bado ana mkataba na Ismailia, amesajiliwa na timu hiyo Januari mwaka huu, tusubiri uongozi utafikia wapi kuhusu dili lake kwani bado wanaendelea kujadiliana,” alisema mtoa taarifa huyo. Usajili wa Poé endapo ukikamilika, basi mchezaji huyo atawapa vitu vingi Simba kutokana na namna mfumo wa Kocha Zoran Maki ataamua kuutumia kulingana na mechi husika kwa sababu ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja eneo la ushambuliaji.
Hivi karibuni, Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez, alisema: “Suala la usajili bado linaendelea, kila ukikamilika tutaweka wazi.” JEAN MOREL POÉ NI NANI? Amezaliwa Desemba 15, 1996, katika Mji wa Abidjan nchini Ivory Coast, kwa sasa ana miaka 25.