Meneja wa klabu bingwa nchini England Liverpool FC Jurgen Klopp, amesema msimu ujao watatumia mbinu za kibabe, ili kutetea ubingwa huo kwa kishindo.
Mabingwa hao wapya wa Ligi Kuu nchini England (EPL) walifanikiwa kutwaa taji hilo juma lililopita, wakisaliwa na michezo saba mkononi, huku wakifanya hivyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 kupita.
Mara ya mwisho kwa Majogoo hao wa Anfield kutwaa ubingwa wa England (Ligi Daraja La Kwanza kwa wakati huo) ilikua mwaka 1990.
Klopp, aliyejiunga na Liverpool mwaka 2015 akitokea Borrusia Dortmund, amesema lengo kuu la klabu hiyo ni kuhakikisha taji la EPL linasalia Anfield, na ana uhakika kazi hiyo itafanikiwa kutokana na kikosi imara atakachokitengeneza baada ya msimu huu.
“Hatutatetea taji msimu ujao, bali tutaushambulia ubingwa kuhakikisha tunaupata, tena kwa kishindo kikubwa”.
“Nimejifunza kitu kwenye ligi hii unapojiona umeshinda basi ndiyo mwanzo wa kushuka kwani kila timu iko vizuri.” Alisema meneja huyo kutoka Ujerumani.
Liverpool wanaongoza msimamo wa ligi ya England (EPL), kwa tofauti ya alama 23 dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili Manchester City, ambayo leo Alhamis itapapatuana na mabingwa hao wapya kwenye dimba la Etihad.
Kuelekea mtanange huo meneja wa Manchester City Pep Guardiola amesema kuwa, watawafanyia gwaride la heshima Liverpool kama sehemu ya kutoa heshima kwao.