Kikosi cha Timu ya Manispaa ya Kinondoni (KMC FC) kimerejea kambini kuendelea na maandilizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/2021, baada ya mapumziko ya siku nne.
Kikosi cha KMC FC kilipata fursa ya kupumzika kwa siku nne, baada ya safari ya Jijini Mwanza Novemba tano mwaka huu, ambapo wakiwa huko walicheza michezo mitatu ya Ligi Kuu dhidi ya Young Africans (CCM Kirumba), Gwambina FC (Gwambina Complex) na Biashara United FC (Uwanja wa Karume-Musoma).
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya KMC FC Christina Mwagala amesema, wachezaji ambao hawajarejea kikosini hadi sasa kwa sababu mbalimbali ni pamoja na Juma Kaseja, David Brayson ambao waliitwa katika timu ya Taifa (Taifa Stars) Hassan Kapalata, Rahim Sheih, Israel Mwenda ambao waliitwa katika kikosi cha Timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), pamoja na Keny Ally ambaye alifiwa na Baba yake mzazi.
“Tumejipanga katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama kwa muda, tuna waandaa wachezaji wetu pindi tutakaporejea, tutahakikisha kuwa tunafanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yetu tukianza na Namungo.
KMC FC inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara chini ya kocha mzawa Habib Kondo, ambaye ameshakiongoza kikosi chake katika michezo kumi, akishinda minne, kufungwa mitatu na kutoka sare mitatu.