Kikosi cha KMC FC tayari kimewasili jijini Dodoma kikitokea Mbarali Mkoani Mbeya kuwakabili Mafande wa JKT Tanzania mchezo utakaopigwa Disemba 23, kwenye uwanja wa Jamuhuri Jijini hapa.
KMC FC ambao watakua wageni katika mchezo huo watakuwa jijini humo kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo, ili kuhakikisha kwamba wanaondoka na alama tatu dhidi ya JKT Tanzania.
Licha ya kwamba KMC FC imepoteza michezo mitatu mfululizo, Makocha John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habibu Kondo wanaendelea kukisuka kikosi hicho cha wana Kino Boys ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha kwamba wanaondoka na alama tatu wakiwa Makao Makuu ya Nchi.
“Hali ya kikosi kwa ujumla iko vizuri, pamoja na kwamba tulipoteza mchezo wetu dhidi ya Ihefu lakini bado tunamatumaini makubwa ya kupata ushindi kwenye mchezo wetu unaofuatia, zaidi pia tunayafanyia kazi makosa ambayo yalifanyika katika mchezo wetu uliopita.”
“Kikubwa ni kwamba hatuzarau Timu, hakuna timu nyepesi katika mchezo, ndio mana tumekuja hapa kufanya maandalizi yetu ya mwisho ambayo yatatuwezesha sisi kuondoka na alama tatu licha ya kwamba tunacheza ugenini, lakini mpira hauna ugeni kikubwa ni kujipanga tu.”
Desemba 19, KMC FC ilicheza na Timu ya Ihefu katika uwanja wa Highland Estate Ubaruku, ambapo awali pia ilicheza na Simba katika uwanja wa Mkapa, Mtibwa Sugar katika uwanja wa Jamuhuri Morogoro na hivyo kupoteza michezo yote.
Imetolewa na
Christina Mwagala.