Klabu ya KMC inatajwa kukamilisha usajili wa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’, Andrew Simchimba, aliyefunga mabao saba msimu uliopita, huku nafasi ya pili akiwa ni Clement Mzize wa Young Africans (6).

Taarifa zinaeleza kuwa Simchimba anatakiwa kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia KMC FC kwa lengo la kuongeza ushindani katika timu hiyo.

Chanzo kutoka ndani ya timu hiyo kimedokeza kwamba mabosi wa KMC FC wanahaha kupata saini ya mshambuliaji huyo baada ya kuvutiwa na huduma yake kwa msimu uliopita hasa kwenye Kombe la ‘ASFC’.

“Simchimba ni mshambuliaji mzuri, kwahiyo tunaamini kabisa akija hapa kila kitu kitakuwa vizuri kwenye eneo letu la ushambuliaji, hawa waliopo ni wazuri, lakini akiongezeka na yeye itapendeza,” kimesema chanzo hicho.

Hata hivyo inaelezwa kuwa mbali na mshambuliaji huyo, KMC FC tayari imekamilisha usajili wa kiungo wa zamani wa Polisi Tanzania, Fred Tangalo na beki wa kati Mbeya City, Juma Shemvuni.

Tangalo anakwenda kuongeza nguvu kwenye eneo la kiungo, huku Shemvuni akitajwa kwenda kuchukua nafasi ya Ibrahim Ame, anayeachwa.

Mrithi wa Bruce Kangwa kutoka Cameroon
Mzee Mangula afichua siri nzito CCM