Michezo ya ligi kuu ya soka Tanznaia bara ambayo jana iliahirishwa, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha katika mikoa ya Dar es salaam, Shinyanga na Iringa imechezwa hii leo.
Jijini Dar es salaam timu KMC iliwakabili maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Tanzania FC), huku Lipuli FC wakipambana dhidi ya Ndanda FC na Mwadui FC wakiikabili Polisi Tanzania.
KMC FC ambayo ilikua haina matokeo mazuri katika michezo ya hivi karibuni, hii leo imezinduka baada ya kupata ushindi wa bao moja kwa sifuri kwenye Uwanja wa Uhuru.
Bao hilo la ushindi kwa KMC limefungwa na kaka wa mshambuliaji wa Aston Villa ya England Mbwana Ally Samatta (Mohamed Ally Samatta), dakika ya 17.
Katika mchezo huo, JKT Tanzania walipata bao lililofungwa na Hassan Mwaterema dakika ya 19, lakini likakataliwa kwa madai ya mfungaji alikuwa ameotea.
Mkoani Iringa kwenye dimba na CCM Samora Lipuli FC ikalazimishwa sare ya mabao matatu kwa matatu dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara.
Mabao ya Lipuli yamefungwa na Paul Nonga dakika ya 14 na 72 na Frank Sekule dakika ya 52, wakati ya Ndanda yamefungwa na Omary Ramadhani dakika ya 22 Vitalis Mayanga dakika ya 48 na 88.
Wilayani Kishapua mkoani Shinyanga, Mwadui FC wameibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Polisi Tanzania Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga.
Mabao ya wachimba madili ya Almasi yamefungwa na Abubakar Kambi dakika ya 27 na Gerrald Mathias dakika ya 90 na ushei, huku la wageni likifungwa na Marcel Kaheza dakika ya 61.