Wachezaji wa KMC FC watapaswa kupambana kufa na kupona kwenye michezo mitatu iliyobaki kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja, huku wakiivimbia Singida Big Stars kuwa hawatoki salama.
Timu hiyo ambayo iliwahi kuwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, haijawa na matokeo mazuri ikiwa nafasi ya 14 kwa kumiliki alama 26 ikibakiza michezo mitatu kujua hatma yake.
Katika mchezo uliopita timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam, ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi Dodoma Jiji na sasa inajiandaa kuwakaribisha Singida Big Stars, mchezo utakaopigwa Mei 12 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Baada ya mpambano huo, timu hiyo itakuwa na kibarua kizito kumalizia michezo yake miwili ugenini dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City, michezo ambayo itaamua kubaki au kushuka daraja.
Kipa wa timu hiyo, Hussein Abel, amesema kwa sasa hawana mechi ndogo na kilichobaki ni kupambana kufa au kupona kuhakikisha wanashinda mechi zilizobaki.
“Kazi ni ngumu sana, lazima tupambane kadri ya uwezo kuona namna ya kuibakiza salama timu ligi kuu, bado hatujakata tamaa na mipango yetu ni kwenye mechi ijayo na Singida BS,” amesema Abel.
Naye Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amesema licha kipindi kigumu walichonacho lakini siyo muda wa kuonesha unyonge bali wanaendelea kujipanga kwa ajili ya michezo iliyobaki.