Klabu ya Simba leo imemsainisha mkataba wa mwaka mmoja, Kocha wake mkuu, Patrick Aussems ambaye mkataba wake wa awali ulikuwa unaelekea kumalizika.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu hiyo, Mohammed Dewji alisimamia zoezi hilo kwa niaba ya Uongozi wa klabu hiyo.
Akizungumzia hatua hiyo ya Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi amesema kuwa mkataba huo unatokana na kazi nzuri aliyoifanya na kuvuka malengo yaliyokuwa kwenye mkataba wake wa awali.
“Mkataba aliousaini ni wa mwaka mmoja ambao tunaamini ataifanya timu kufika mbali zaidi ya msimu uliopita katika mashindano yote kwani mkataba huu mpya una malengo zaidi ya ule wa msimu uliomalizika,” alisema Mkwabi.
“Tutafanya maandalizi mazuri kuanzia katika Pre-Season kwa kupata mahala sahihi ambapo kila mchezaji ataandaliwa katika njia sahihi. Lakini pia tutafanya usajili wa kuongeza nguvu katika timu kulingana na mapungufu ambayo yalijitokeza katika misimu iliyopita,” aliongeza.
Kocha Aussems ambaye ni raia wa Ubelgiji alivuka malengo yaliyokuwa yameainishwa kwenye mkataba wake wa awali ambao ulimtaka kuipeleka timu hiyo katika hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Afrika lakini yeye aliifikisha hatua ya robo fainali.
Pia, alifanikiwa kuwapa ubingwa wa Tanzania Bara kama alivyotakiwa kwenye mkataba wake.
Simba wanatarajiwa kukabidhiwa Kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara, Jumatano ya wiki ijayo mkoani Morogoro watakapoenda kukipiga na Mtibwa Sugar.