Mshambuliaji wa klabu ya Genk na nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema kuwa atajitahidi kwa uwezo wake wote kuongoza vyema Taifa Stars katika michuano ya mataifa ya Afrika, AFCON mwezi ujao nchini Misri.

Amesema hayo jijini Dar es salaam mara baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere alfajiri ya leo na kupokewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akitokea nchini Ubelgiji katika klabu yake ya Genk.

Samatta ambaye ameonyesha kiwango cha juu msimu huu katika michuano ya Europa League na Ligi Kuu nchini Ubelgiji, amesema kuwa anafahamu jukumu ambalo Watanzania wamewakabidhi kuelekea michuano ya AFCON na yeye kama nahodha na wachezaji wenzake wameahidi kuwa watapambana hadi mwisho.

“Baada ya muda mrefu sana tumepata nafasi hii ya kwenda kushiriki, ukweli ni kwamba ni uzoefu mkubwa sana tunakwenda kuupata kutokana na uchanga wa timu yetu ya taifa kwa sababu hatujakuwepo kwenye mashindano kwa muda mrefu,”amesema Samatta

Aidha, amesema kuwa mpira siku zote una matokeo ya kushangaza, inawezekana Taifa Stars ikawa changa kwasababu ya muda mrefu wa kutoshiriki lakini inawezekana ikafanya vizuri kuliko timu ambazo zimepewa nafasi kubwa.

Hata hivyo, Samatta amezungumzia juu ya ndoto yake ya kucheza soka nchini Uingereza, ambapo amesema, “huwezi jua kinachokuja mbele lakini mimi siku zote toka nikiwa mtoto tulikuwa tunaenda kwenye mabanda ya kuonyesha mpira na nilikuwa mmoja wapo ambaye nilikuwa napenda kuangalia EPL, ni kitu ambacho kinanivutia sana. Napenda kucheza ligi ya Uingereza lakini huwezi jua itakuwaje,”amesema Samatta

Kocha Aussems aongezewa mwaka mmoja kuinoa Simba
Dhahabu ya bilioni 34.3 yauzwa kwa kipindi cha mwezi mmoja

Comments

comments