Uongozi wa Klabu ya Mashujaa FC itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao 2023/24, umemtangaza Mohamed Abdallah ‘Bares’, kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua nafasi ya Abdul Mingange, aliyeipandisha daraja.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ya mkoani Kigoma imesema kuwa kocha huyo atakinoa kikosi hicho kikiwa kinacheza ligi hiyo kwa mara ya kwanza.
Awali, Bares alikuwa kocha wa Tanzania Prisons ambapo aliiwezesha timu hiyo iliyokuwa inashika mkia kwenye Ligi Kuu kumaliza ikiwa ya nane msimu uliomalizika.
Akizungumza baada ya kutambulishwa, Bares aliyepewa mkataba wa mwaka mmoja, amesema kazi iliyobaki ni kufanya usajili bora ili timu hiyo iweze kufikia malengo yake.
“Nashukuru Mungu, niko tayari kufanya kazi kwenye klabu ya Mashujaa, najisikia vizuri kwa sababu mimi ni mwalimu wa mpira, timu yoyote naweza kufundisha, nimekuja huku kwa ajili ya kazi kuifikisha sehemu ambayo tunayoihitaji,” amesema kocha huyo ambaye alichukuliwa na Prisons akitokea Mlandege ikiwa ni baada ya kuipa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka huu.
Amesema yeye kama Kocha Mkuu, atajipanga na benchi lake la ufundi kutengeneza kikosi cha ushindani, huku akiwataka mashabiki wa Mashujaa FC kuendeleza moto ule ule waliouonyesha wakati timu hiyo ikisaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu.
“Kwanza niwapongeze kwa kupanda Ligi Kuu, kingine ni kwamba waendelee kuisapoti timu yao kama walivyofanya wakati wa mapambano ya kuipandisha daraja, kwa upande wetu sisi tumejipanga vizuri kama benchi la ufundi kuona timu yao inafanya vizuri.
“Wakumbuke nao ni wachezaji wa 12, ushirikiano wetu, viongozi na mashabiki ndiyo utatufikisha kule ambako tunataka tufike na kwa upande wa kikosi tutafanya usajili mzuri na wa kuvutia, ila ikumbukwe wachezaji ni wale wale tu, ni kiasi cha kutoa kule na kumleta hapa, kinachohitajika atengenezwe na yeye mwenyewe ajitume awe msaada kwenye timu,” amesema kocha huyo.
Mashujaa ilikuwa timu ya tatu kupanda daraja msimu huu kutoka Ligi ya Championship, ikiiondoa Mbeya City kwenye mechi ya ‘Play Off’ kwa kuitwanga Mbeya City jumla ya mabao 4-1 kwa mechi za nyumbani na ugenini.