Uongozi wa Klabu ya Tanzania Prisons umethibitisha kumuajiri Kocha Abdallah Mohamed Juma ‘Bares’ baada ya kukamilisha mazungumzo yaliyodumu kwa siku kadhaa.
Bares amekamilisha mpango wa ajira klabuni hapo, akitokea Visiwani Zanzibar, ambako ameiwezesha Klabu ya Klabu ya Mlandege Kutwaa Ubingwa wa Mapinduzi 2023 kwa kuifunga Singida Big Stars 2-1.
Taarifa iliyosambazwa na Tanzania Prisons katika Mitandao ya Kijamii imeeleza kuwa, Klabu hiyo imesaini mkataba wa mwaka mmoja na Kocha huyo, ambaye rasmi anaanza kazi mara moja.
“Uongozi wa timu unaimani kubwa na Kocha na tunaamini atatupa kile ambacho Uongozi unakitarajia kutoka kwake.” imeeleza taarifa hiyo
Wakati huo huo Kocha Msaidizi wa Tanzania Prisons Shaban Mtupa amewaondoa hofu mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo, ambao wamepoteza imani na timu yao, wakiamini huenda ikashuka daraja mwishoni mwa msimu huu.
Mtupa ambaye alikua akikaimu nafasi ya Kocha Mkuu amesema Kikosi chao kipo imara na tayari kwa mapambano yaliyosalia msimu huu, na wanaimani watafanya vizuri na kusalia Ligi Kuu kwa msimu ujao.
“Vijana wetu wapo tayari, tumekua na mipango mikubwa na mizuri ili kuhakikisha tunashinda michezo yetu iliyosalia msimu huu, kila mchezaji anaonesha kujituma.”
“Tunakiri Ligi Kuu imekua na ushindani mkubwa zaidi msimu huu, lakini hilo halituzuii kufanikisha tunachokikusudia, hivyo niwatoe waswasi Mashabiki wa Tanzania Prisons, wanachotakiwa ni kuendelea kutuombea na kutushangilia kila tunapokua kwenye majukumu ya kusaka alama tatu.” amesema Mtupa.
Tanzania Prisons itachezas dhidi ya Mtibwa Sugar keshokutwa Ijumaa (Februari 03), katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Tanzania Prisons inamiliki alama 21 zinazoiweka nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu, ikishinda michezo mitano , sare sita na kupoteza mara kumi.