Ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC FC umemfanya Kocha Mkuu wa Coastal Union Juma Mgunda akimwagie sifa kikosi chake, ambacho kimesheheni idadi kubwa ya Wachezaji waliosajili msimu huu.
Coastal Union ni moja ya Klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizopoteza Wachezaji wengi kwa kusajiliwa na klabu nyingine zinazoshiriki Ligi hiyo, na Wadau wengi waliamini huenda ingeanza vibaya msimu kutokana na Wachezaji wengi kuwa wapya.
Akiwa katika Mazungumzo ya kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans, utakaochezwa kesho Jumamosi (Agosti 20) katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Kocha Mgunda amesema hana budi kujipongeza na kuwapongeza Wachezaji wake.
Amesema Coastal Union ilipitia wakati mgumu baada ya kuondokewa na Wachezaji wake Saba ambao wamesajiliwa na klabu nyingine za Tanzania Bara, lakini kwa kushirikiana na Benchi lake la Ufundi wamefanya kazi kubwa kujenga Umoja na Mshikamano kwa Wachezaji wapya na wale waliobaki kikosini, na walifanikiwa kupata matokeo.
“Katika Makocha ambao waliingia kwenye Mtihani mkubwa mwishoni mwa msimu uliopita basi mimi ni mmoja wao, Wachezaji karibu Saba waliondoka kwenye timu, ikatulazimu kuwasajili Saba wengine ambao wameziba nafasi zao.”
“Haikuwa rahisi kwangu na Benchi langu la Ufundi kufanya kazi ya kuwaandaa kabla ya kuanza kwa msimu mpya, ninamshukuru Mungu tulianza vizuri kwa kuifunga KMC FC, kwa hakika sifa pekee za awali ziende kwa Wachezaji ambao walipambana kwa kufuata maelekezo.”
Katika hatua nyingine Mgunda amesema Kikosi chake kilichosheheni sura mpya kesho Jumamosi (Agosti 20) kitakua na Mtihani mwingine wa kuikabili Young Africans kikiwa nyumbani Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
“Tunakwenda kwenye Mtihani wa pili baada ya kushinda Mtihani wa kwanza dhidi ya KMC FC, tunajua Young Africans wamejiandaa kukabiliana na sisi, lakini kazi ipo pale pale ya kuhakikisha tunapambana na kuendelea kuonyesha Umoja na Mshikamano wetu kesho Jumamosi (Agosti 20)” amesema Mgunda.
Wawili hao kwa mara ya mwisho walikutana Uwanjani hapo katika mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na kuambulia matokeo ya sare ya 3-3, kabla ya sheria ya Matuta kuchukua mkondo wake na kuibeba Young Africans.