Wakati msimu mpya wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) ukitarajiwa kuanza mwezi ujao tambo na majigambo yameanza mapema kwa kocha wa Dar City, Mohamed Mbwana kuzitisha timu shiriki akidai watachukua wachezaji muhimu wanaoshiriki ligi hiyo.
Mbwana aliyewahi kuinoa Pazi kwa mafanikio, amedai lengo lao ni kusajili wachezaji wenye ubora.
“Kama tulisajili wachezaji wa kimataifa kutoka nchi za Kenya na Sudan tukiwa Daraja la Kwanza, naamini hatutasumbuka kubeba wachezaji wazawa ili waichezee Dar City katika RBA msimu huu,” amesema Mbwana aliyetamba kuchukua baadhi ya mastaa kutoka Pazi.
Kocha huyo amesema majina ya kikosi yatawekwa hadharani siku mbili kabla ya kuanza kwa ligi ambapo Kamishna wa Ufundi na Mashindano, Haleluya Kavalambi amesema RBA itashirikisha timu 16 za wanaume na 12 za wanawake.
“Timu za wanaume zimeongezeka kutoka 15 hadi 16 na wanawake kutoka timu saba hadi 12. Kuongezeka huku ni moja ya mafanikio ya maendeleo ya mchezo wa kikapu Mkoa wa Dar es Salaam,” amesema Kavalambi.
Amezitaja timu shiriki kuwa ni Pazi, ABC, Oilers, Chui, Dar City, Polisi, Don Bosco Oysterbay, Savio, JKT, UDSM Outsiders, Jogoo, Ukonga Kings, Mchenga, Ukonga Warriors, Mgulani JKT na Vijana City Bulls.
Wanawake ni Don Bosco Lioness, JKT Stars, Jeshi Stars, Kurasini Divas, Mchenga Queens, Pazi Queens, Ukonga Queens, City Queens, UDSM Queens, Polisi Stars na Oilers Princeses.