Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya England Gareth Southgate amesema hana budi kuiwezesha timu yake kufanya vizuri kwenye Fainali za Mataifa ya Ulaya ‘EURO 2024’, ili kuweka mazingira mazuri ya ajira yake.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 52amekuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la England tangu mwaka 2016, akichukua mikoba baada ya kufukuzwa kwa Sam Allardyce.
England ilitinga Nusu Fainali ya Kombe la Dunia 2018 kabla ya kupoteza mchezo wa fainali ya Euro 2020 kwa mikwaju ya Penalti na Italia kwenye uwanja wa Wembley.
Kulikuwa na dalili zaidi za maendeleo wakati timu hiyo ilipotolewa nje na Ufaransa kwenye Kombe la Dunia mwaka jana, lakini mwaka mgumu ulimfanya Southgate afikirie kama atamaliza mkataba wake hadi 2024.
Kocha huyo aliamua kusalia baada ya juma moja ya kutafakari kufuatia kufanya vibaya Qatar, lakini michuano ya Ulaya msimu ujao inaweza kuthibitisha fainali zake za mwisho kuinoa England. “Mkataba wangu ni hadi Desemba,” amesema Southgate.
Mtazamo wa haraka wa England ni kuchukua hatua kubwa kuelekea Ujerumani kwa kuzishinda Malta na Macedonia Kaskazini mnamo Juni, lakini kwa wachezaji kadhaa mustakabali wao uko hewani.