Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliveira, ameweka wazi kuwa licha ya kupokea ofa nyingi kutoka klabu za nje ya nchi, amezikataa na amejipanga kuiandaa Simba itakayokuwa na makali yatakayowawezesha kutwaa makombe mbalimbali.

Robertinho amesema bado hajamaliza kazi yake ndani ya Simba SC na lengo lake ni kuisuka timu hiyo na kuifanya kuwa tishio ndani na nje ya Tanzania.

Kocha huyo amesema kwa sasa timu yake inahitaji mabadiliko makubwa na pia fikra za wachezaji zinatakiwa zibadilike kwani amegundua kuwa Simba ni klabu kubwa sana Barani Afrika.

“Simba SC ni timu kubwa lakini tunahitaji nini? Kwa wakati huu tuibadili timu yetu, tunatakiwa kubadili mipango yetu, fikra za wachezaji, nadhani sasa ni muda mzuri wa kuandaa timu yetu, inabidi tuandae timu imara, kuna ofa nyingi zimekuja kwangu lakini nimeamua kubaki hapa, napenda kila kitu nina furaha kwa ajili ya watu wa Tanzania, wanapenda sana mpira na wanapenda timu yao, baada ya kupokea maombi mengi nimeamua kubaki hapa nataka nibaki nitengeneze kikosi kizuri na cha kutisha kitakacholeta upinzani mkubwa Afrika,” amesema

Amesema lengo lake ni kutengeneza kikosi kitakachokuwa na wachezaji wawili wawili kwenye kila nafasi huku wakiwa na uwezo sawa kwani kwa sasa wasipokuwapo baadhi ya wachezaji, timu inapwaya.

“Nataka kila nafasi iwe na wachezaji angalau wawili ambao hawapishani sana, kama Saido hachezi, Mzamiri kama hachezi, wawepo wachezaji wengine kama wao wanaoweza kuanza kwenye kikosi, Simba SC inatakiwa iwe na kikosi imara, kwa sababu ni timu kubwa inayozungumzwa sana, hata  Misri, Morocco, Tunisia kote wanaizungumzia,” amesema kocha huyo mwenye umri wa miaka 62.

Mipango na maneno ya kocha huyo inafanana sana na maoni ya wanachama na mashabiki wa Simba SC kuwa kikosi chao ni finyu, kina wachezaji wachache wenye uwezo wa hali ya juu kiasi cha kuweza kupambana na klabu yoyote Afrika na kushinda, lakini nusu ya kikosi kilichobaki ambacho kingewasaidia wenzake kina wachezaji ambao huenda wasiweze hata kuingia nne bora ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Msimu huu Simba SC imetoka kapa katika kila mashindano waliyoshiriki, kwa mara ya pili mfululizo wameshuhudia ubingwa wa ligi kuu ukienda kwa wapinzani wao wakubwa Young Africans, lakini wameondolewa kwenye hatua ya Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la TFF (ASFC) huku pia wakiishia hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

TARURA yaanza utekelezaji agizo la Chongolo
Gareth Southgate ashtuka England