Kocha Mkuu wa Ihefu FC, John Simkoko ametamba kuifunga Simba SC katika michezo yote miwili watakazokutana mwezi April.
Michezo hiyo miwili, wa kwanza ni ule wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utachezwa katika Uwanja wa Highland Estate, mkoani Mbeya na mchezo wa pili ni wa hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ ambao utapigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kocha huyo mkongwe ameeleza kuwa kuimarika kwa kikosi chake ndio kunampa matumaini ya kuibuka na ushindi ingawa ametamba kuwa michezo yote miwili itakuwa migumu.
“Tuna kikosi imara chenye wachezaji wazoefu kama ilivyo kwa Simba SC, lakini pia tuna malengo ya kufika mbali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa hiyo Simba wajiandae sababu wanakutana na Ihefu yatofauti kabisa,” amesema Simkoko.
Kocha huyo amesema mipango yao ni kutochafua rekodi ya kuzifunga timu kubwa kwenye uwanja wao wa nyumbani baada ya kuzifunga timu za Young Africans, Mtibwa Sugar na Azam FC hivyo haoni kama kuna sababu ya Simba SC kuepuka kichapo hicho.
Amesema kila mchezaji ndani ya kikosi chake anasubiri kwa hamu michezo hiyo miwili na hawatacheza kwa kukamia bali watacheza mchezo wao wa kawaida wakilenga kupata ushindi kama inavyokuwa kwenye michezo mingine.
Ihefu FC ambayo ilimaliza mzunguko wa kwanza ikishika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa sasa ipo nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi hiyo ikiwa na alama 33 na kuna uwezekano ikamaliza Ligi ndani ya timu tano bora kutokana na idadi michezo waliyobakiwa nayo.