Kocha Mkuu wa Kipanga FC ya Zanzibar Hassan Abdulrahman Said ameipa ushauri wa bure Young Africans kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza Hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans itakua mwenyeji wa mchezo huo kesho Jumatano (Novemba 02), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikihitaji kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri, kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili utakaopigwa mjini Tunis-Tunisia Novemba 09.
Kocha Hassan ametoa ushauri huo kufuatia kikosi chake kuonja chachu na chungu ya kucheza na Club Africain katika Hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Kipanga FC ilianzia nyumbani Uwanja wa Aman kisiwani Unguja-Zanzibar na kuambulia sare ya 0-0, kisha ilipokwenda Tunisia ilichezea Bakora 7-0, na kutupwa nje ya Michuano hiyo.
Kocha Hassan amesema walikutana na mazingira magumu sana walipofika nchini Tunisia, licha ya kupokelewa kwa ukarimu na wenyeji wao, ambao walikua wakiwasubiri Uwanja wa Ndege.
Amesema jambo kubwa ambalo lilianza kuwaondoa mchezoni ni kunyimwa nafasi ya kufanya mazoezi kwenye Uwanja walioutumia siku ya mchezo, na badala yake walipelekwa kwenye Uwanja mwingine, hivyo amewataka Young Africans kuwa tayari kwa sakata hilo endapo litawafika.
“Hatukupewa nafasi ya kufanya mzoezi katika Uwanja tulioutumia siku ya mchezo, tulipelekwa kwenye Uwanja mwingine, kilichofanywa na wenyeji wetu walitupeleka kutembelea Uwanja ambao tuliutumia siku ya mchezo ili kuutazama tu, na tulipowataka tufanye mazoezi hata kwa dakika chache walitukatalia.” amesema Kocha Hassan
Hata hivyo Kocha Hassan amesema anaamini Young Africans ni timu Kubwa na Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo wanakwenda kukutana na Wakongwe wenzao kwenye Michuano mikubwa Barani Afrika, hali ambaho italeta upinzani patashika nguo kuchanika.
Amesema kinachotakiwa kufanywa na Young Africans ni kucheza kama hawaifahamu Club Africain, ambayo msimu huu imewahi kuja Tanzania na kucheza na Kipanga FC huko visiwani Zanzibar.
“Natambua Young Africans wana uwezo wa kupambana na huenda wakawafunga hapo na hata kwao, lakini ninachowasihi wasichukulie kama wanaifahamu sana Club Africain, kwa kigezo iliwahi kucheza na Kipanga FC ya Zanizbar, hilo waliondowe katika vichwa vyao.”
“Club Africain ni klabu yenye mbinu nyingi sana, kwa hiyo nayo itakuja na mfumo tofauti kabisa na ilivyokuja awali kucheza na sisi, hivyo Young Africana wawe makini sana katika mchezo wao wa kesho Jumatano.” amesema Kocha Hassan