Beki wa Young Africans, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ amesema lilikuwa ni suala la muda kwake kupata nafasi na kuonyesha kile alichonacho huku akiweka wazi siri ya ubora wake ndani ya dakika alizopata kucheza kuwa ni kutokukata tamaa na kuonyesha mazoezini.

Bacca amecheza mechi mbili mfululizo dhidi ya Simba akianzia benchi alicheza dakika 45 na amepata nafasi ya kucheza dakika 90 dhidi ya Geita Gold iliyokubali kufungwa 1-0 nyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bacca alisema alisajiliwa Young Africans ili acheze anashukuru Mungu muda wake sasa umefika nafasi aliyoipata hatamani kukosea hata sekunde moja kwani bado anahitaji muda zaidi ili kuonyesha kile alichonacho mguuni huku akiweka wazi kuwa kuto kuonyesha tofauti kwa benchi la ufundi na wachezaji ndio kitu pekee kilichompa nafasi ya kuwa bora.

“Lilikuwa ni suala la muda tu kuingia uwanjani na kucheza nafurahi sasa umetimia kujituma kwenye uwanja wa mazoezi kukubali kujifunza na kukaa vizuri na wachezaji wenzangu na benchi la ufundi ni kitu pekee ambacho kimenifanya niwe bora na kupata ushirikiano mzuri,” alisema na kuongeza;

“Kila mchezaji aliyesajiliwa Yanga ana nafasi ya kucheza kujituma kuamini katika muda ndio kitu pekee kinaweza kumfanya mchezaji yeyote akawa bora hatakiwi kubweteka na kukubali kuwa hana nafasi ata siku akipewa nafasi ya kucheza hawezi kuonyesha ubora.” alisema.

Alisema anaheshimu ubora wa wachezaji wote wanaocheza nafasi anayocheza kikubwa kilichompa namba ni juhudi zake binafsi na anatamani kuona anapata namba ya kudumu kikosi cha kwanza ili aweze kuendelea kuwa bora zaidi ya alipo sasa.

Bacca alisema anafurahishwa na uchezaji wa wachezaji wote hana chaguo na anawaheshimu kutokana na kujifunza vitu vingi kutoka kwao kutokana na uzoefu walionao anatamani siku moja na yeye aaminiwe kwenye kiklosi cha kwanza kwa kupewa muda mwingi wa kucheza.

Beki huyo alisajiliwa na Young Africans dirisha kubwa la usajili kwa mkataba wa miaka miwili akitokea KMKM ya Zanzibar ambao ni mabingwa watetezi msimu huu baada ya kutwaa taji la Ligi msimu ulioisha.

Chanzo: Mwanaspoti

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Novemba 1, 2022     
Nabi afunguka ubora wa Club Africain