Kocha Mkuu wa klabu ya soka ya KMKM, Ame Msimu, ameushukuru uongozi wa Young Africans kuwaalika jijini Dar es salaam, kwa ajili ya mchezo wa kirafiki utakaochezwa leo usiku kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Young Africans watautumia mchezo huo kama sehemu kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Unoin, utakaochezwa Jumamosi, Oktoba 03 Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha Ame amesema wamepata mwaliko wa kucheza mchezo huo na wameukubali, huku akiamini utakisaidia kikosi chake kujiimarisha kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zanzibar, ambao utaanza Novemba 07.
Kocha huyo amesema kikosi chake kiliwasili jana Jumanne jijini Dar es salaam kikiwa na wachezaji 26, huku akimtaja mshambuliaji, Mussa Ali Mbarouk, kuwa atakosekana kwenye mchezo huo kwa sababu ni majeruhi.
“Tuliwasili Dar es salaam jana, tumekuja na wachezaji wetu wote tuliowasajili, isipokuwa Mbarouk ambaye alipata majeraha ya mguu akiwa mazoezini,” amesema kocha Ame.
Amesema anatarajia kuwatumia wachezaji wake wote ili kuwajenga na kuwapa uzoefu dhidi ya Young Africans ambayo ni timu kongwe na yenye wachezaji wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali.
“Wenzetu ni wazoefu na wana wachezaji wazuri, ila lengo letu kwa pamoja ni kuhakikisha timu inacheza vizuri na kukiandaa kikosi chetu kuelekea michezo ya Ligi Kuu Zanzibar ambayo msimu huu itakuwa na ushindani zaidi,” Amesema.
Aliongeza kuwa, baada ya kumaliza mchezo huo, kikosi chake kitarejea kisiwani Unguja (Zanzibar), kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Zanzibar, sambamba na kucheza michezo mingine ya kirafiki.