Hatimaye Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ limetangaza adhabu kwa Kocha wa Makipa wa Mashujaa FC, Shomari Ndizi, ambaye alimpiga ngumi Kocha Mkuu wa Mbeya City wakati wa mchezo wa Mkondo wa Pili wa ‘Play Off’ uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita mjini Mbeya.
Tukio hilo lilitokea wakati wachezaji wa akiba na maofisa wa benchi la ufundi la Mashujaa FC wakishangilia bao pekee katika mchezo huo, ambao uliiwezesha timu hiyo ya mkoani Kigoma kupanda Ligi Kuu, ikitokea Championship.
TFF imetangaza kumfungia Shomari Ndizi kushiriki ligi na mashindano yaliyo chini ya Shirikisho hilo kwa msimu wa 2023/2024 na kumtoza faini ya Sh 2,000,000 kwa kosa la kumpiga ngumi Kocha Mkuu wa Mbeya City, Abdallah Mubiru.
Afisa Habari wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Karim Boimanda amesema: “Kamati ya saa 72 ilipitia mwenendo wa ligi na kufanya maamuzi hayo, pamoja na adhabu hiyo ya kocha pia Mashujaa imetozwa faini ya shilingi 500,000 kwa kosa la kukataa kutumia chumba cha kuvalia nguo kwenye Uwanja wa Sokoine,”
Pia Mbeya City imetozwa faini ya Sh 2,500,000 ambapo Sh 1,000,000 ni kwa mashabiki wake kuwapiga na kuwasababishia majeraha mashabiki wa KMC, Abdul Mohamed na Seif Membe na Sh 500,000 kwa kosa la waokota mipira kuchelewa kwa makusudi kurejesha mipira uwanjani.
“Membe alikwenda kumuokoa Mohamed aliyekuwa akipigwa na mashabiki wa Mbeya City na kujikuta wote wanapata majeraha.
Katika tukio hilo, Membe alipoteza simu ya mkononi yenye thamani ya Sh 480,000 na Sh 220,000, kamati imeiadhibu City kulipa gharama ya simu na fedha hizo,” amesema.
Aidha, klabu ya Young Africans nayo imetozwa faini ya Sh 1,000,000 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa walinzi wa uwanjani wakati wa mchezo dhidi ya Mbeya City, nayo Mbeya City imetozwa Sh 1,000,000 kwa kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa wachezaji wa Young Africans.