Kocha wa Walinda Lango wa Mbeya City FC Ally Mustapha ‘Bartez’ amewatoa wasiwasi Mashabiki wa Klabu hiyo, kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC.
Mbeya City itakua mgeni wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, keshokutwa Jumatano (Januari 18), mishale ya saa moja usiku.
‘Bartez’ amesema baada ya kuangukia pua mbele ya Azam FC mwishoni mwa mwaka 2022 kwa kufungwa 6-1, wamejitathmini na kutambua makosa yao, hivyo wamejiandaa vizuri ili kufanya vizuri dhidi ya Simba SC.
Amesema upande wa Walinda Lango wapo vizuri na wataonesha umahiri mkubwa kwenye mchezo huo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Soka nchini Tanzania, baada ya kukosa burudani ya Ligi Kuu kwa muda wa majuma mawili.
“Kwa upande wa golini sina wasiwasi kabisa, tumefanyia kazi makosa tangu tulipomaliza mchezo wetu na Azam FC, hivyo Simba SC isitarajie mteremko.”
“Tunaenda kufanya kweli na kuwapa raha mashabiki wa Mbeya City.” amesema Ally Mustafa ‘Bartez’
Mchezo wa Duru la Kwanza uliozikutanisha timu hizo, ulishuhudia Mbeya City ikisawazisha dakika za mwisho, na kupelekea kugawana alama, katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.