Saa kadhaa zikisalia kabla ya Nusu Fainali ya Pili ya Kombe la Dunia kupigwa nchini Qatar, Kocha Mkuu wa Timu ya taifa ya Morocco Walid Regragui, amefunguka namna Mataifa ya Barani Ulaya yanavyochukizwa mafanikio ya Afrika.
Kocha Regragui ameweka historia ya kuifikisha timu ya Afrika Nusu Fainali kwa mara ya kwanza katika Fainali za Kombe la Dunia, akivunja Rekodi ya Cameroon, Senegal na Ghana zilizofika Robo Fainali.
Kocha huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa, Mataifa ya Barani Ulaya yamekua yakichukizwa na Mafanikio ya Bara la Afrika na hatua waliofikia Morocco imekua kama kero kwao.
Amesema sumu hiyo ya Chuki inabebwa na kusabazwa na Waandishi wa Habari wa Barani Ulaya, lakini kwa sasa wameona namna ambavyo Afrika imebadilika na kupiga hatua kubwa katika mchezo wa Soka.
“Waandishi wa habari wa Ulaya hawapendi timu za Kiafrika kucheza kama Wazungu, zamani timu za Kiafrika zilionekana kama timu zilizocheza kwa ajili ya kujifurahisha lakini hazikuwa na ufanisi.
“Tuna tamaa kubwa, tuna njaa. Kujiamini na kuamua kuandika upya vitabu vya historia. Tunataka Afrika iwe juu zaidi duniani.” amesema Walid Regragui
Kikosi cha Morocco leo Jumatano (Desemba 14) kitakua kinasaka Rekodi nyingine katika Fainali za Kombe la Dunia mbele ya Mabingwa Watetezi Ufaransa katika mchezo wa Nusu Fainali.
Mshindi wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Al Bayt, mjini Al Khor, atakutana na Argentina kwenye mchezo wa Fainali Jumapili (Desemba 18), katika Uwanja wa Lusail, mjini Lusail nchini Qatar.