Kocha Mkuu mpya wa Coastal Union, David Oumna ameahidi kuirudisha timu hiyo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24.

Ouma amejiunga na timu hiyo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea kwao Kenya alipokuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ‘Harambee Stars’.

Oumna amesema kinachompa matumaini ni ubora wa wachezaji wengi wa timu hiyo pamoja na vipaji walivyonavyo.

“Nimevutiwa na vitu vingi kwa muda mfupi tangu nimejiunga na Coastal, kikubwa ni uwezo wa wachezaji, wengi wana umri mdogo na ni wapambanaji naamini nikiongeza mbinu zangu tutakuwa miongoni mwa timu zinazopigania ubingwa msimu huu,” amesema Ouma.

Pia amesema anajua hawapo katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi lakini malengo yake ni kutumia mapumziko ya kalenda ya FIFA, kukiimarisha kikosi hicho ili ligi itakapoendelea waweze kupata matokeo mazuri.

Amesema baada ya kutambua uwezo wa wachezaji atakachokifanya ni kumkabidhi jukumu kila mchezaji ili kuhakikisha wanatimiza malengo ambayo wamekusudia kuyafikia msimu huu 2023/24.

Coastal Union ipo nafasi ya 13 kwenye msimamo, ikikusanya pointi saba katika michezo tisa iliyocheza huku ikishinda mchezo mmoja, imefungwa michezo minne na kutoka sare mechi nne.

Raphinha kuwekwa sokoni Januari 2024
Steven Gerrard amuwashia moto Al-Kuwaykibi