Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar Zuberi Katwila amesema ana kazi kubwa ya kuboresha safu ya ulinzi ya timu hiyo ili mambo yaende sawa katika Michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2023/24.
Mtibwa Sugar imeendelea kufanya vibaya msimu huu, ikipoteza michezo minne mfululizo hali ambayo inaendelea kuifanya timu hiyo ya mkoani Morogoro kuendelea kuburuza mkia wa msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa.
Mchezo wa mwisho kwa timu hiyo ilishuhudiwa ikipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Tabora United, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora hali ambayo imemuibua Kocha Mkuu Katwila ambaye amekiri ana kazi kubwa ya kufanya.
Kocha huyo mzawa amesema hazungumzi hayo kwa ajili ya kulaumu isipokuwa kama kocha wamezibeba kasoro hizo na ameanza kuzifanyia marekebisho.
“Soka ndio lilivyo wakati mwingine lakini kufungwa sio kuzuri, haina mwendelezo mzuri kwetu, ila sasa tuna kazi kubwa ya kufanya ili kutengeneza ulinzi mzuri, tusifungwe tupate uwiano mzuri na hii sio sehemu ya kulaumiana ila kama makodha tumeliona hilo na kazi yetu ni kurekebisha,” amesema Katwila
Amesema pamoja na kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Tabora United, kuna mabadiliko ameyaona ndani ya kikosi yanayoleta mwanga mzuri, akiamini watakaa sawa muda si mrefu na wataondokana na presha ya kupoteza waliyonayo sasa.