Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar Awadh Juma amesema kikosi chao kimewasili salama jijini Dar es salaam tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans.
Kesho Jumanne (Septemba 13) Young Africans itakuwa wenyeji wa mchezo huo Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiendelea kujidaia rekodi ya kutopoteza mchezo wa Ligi Kuu tangu msimu uliopita.
Awadh Juma amezungumza na waandishi wa Habari leo Jumatatu (Septemba 12) Mchana na kueleza maandalizi yao kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans, ambao amekiri ukutawa na upinzani mkubwa.
Amesema wanafahamu Young Africans wana kikosi bora na imara, lakini akasisitiza kuwa hata wao msimu huu wana kikosi kizuri ambacho kimeanza vyema msimu na hadi sasa hakijapoteza mchezo.
“Tunawaheshimu sana Young Africans, tunafahamu wana timu nzuri na nsio maana hadi sasa hawajapoteza mchezo tangu walipoanza msimu huu, na sisi hatujapoteza mchezo, ninaamini utakuwa mchezo wenye ushindani na burudani”
“Soka lina historia sikatai, lakini hata sisi tumewahi kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, kwa hiyo ni jambo la kawaida, wao ni mabingwa kwa wakati huu na sisi tuliwahi kuwa mabingwa kwa wakati wetu, kikubwa hapa ni kwenda kupambana kesho, ili kupata alama tatu muhimu.” amesema Awadh Juma ambaye aliwahi kuitumikia Mtibwa Sugar kama mchezaji.