Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said leo Jumatatu (Septemba 12), amesaini mkataba mpya wa udhamini na kampuni ya GSM wenye thamani ya Shilingi Bilioni 10.9 kwa miaka mitano.

Mkataba huo uliogawanyika sehemu mbili utahusisha, mkataba wa kwanza wa uzalishaji na usambazaji wa jezi pamoja na bidhaa mbalimbali za klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ambapo kila mwaka GSM Group itailipa Young Africans Shilingi Bilioni 1.5 ambayo itakua inaongezeka kwa 10% na kufanya jumla ya thamani kuwa Shilingi Bilioni 9.15 ndani ya miaka mitano.

Mkataba wa pili utakua ni wa udhamini, ambapo GSM italipa Shilingi Milioni 300 kwa mwaka itakayokuwa ikiongezeka kwa 10% kila mwaka kwa muda wa miaka 5 kuifanya jumla kuwa na Shilingi Bilioni 1.83 kwa miaka mitano.

Akizungumzia makubaliano hayo mbele ya waandishi wa habari, Rais wa klabu ya Young Africans Injiniaa Hersi Said amesema: “Tunayo furaha kubwa kuingia makubaliano haya mapya na wenzetu wa GSM, moja ya ajenda zangu katika uongozi wangu ilikuwa ni kuipa klabu uimara wa kiuchumi ili tuweze kujitegemea.”

“Na mikataba kama hii inaiongezea klabu thamani na kuiimarisha kimapato, na kama tujuavyo uendeshaji wa vilabu vyetu kunahitaji uiamara wa kiuchumi”

“Niwapongeze kampuni ya GSM kwa kuendelea kuwekeza katika klabu yetu uwekezaji wa namna hii sio tu kunaongeza thamani timu yetu bali inasaidia kwa namna nyingine kukuza soka nchini kwetu kwa ujumla”

“Niwaombe na Wanachama wa Young Africans SC waendelee kuiunga mkono kampuni ya GSM kwa kunununa bidhaa na huduma zao ili waendelee kunufaika na udhamini wao kwetu”

Kwa upande wa mdhamini, Mkurugenzi wa Biashara kutoka GSM Group Allan Chonjo amesema: “GSM imeona matunda makubwa sana baada ya kuingia mkataba na Klabu kubwa ya Young Africans na hivyo tumevutiwa na kuamua kuendelea kuwekeza kwa kipindi cha miaka 5 kuanzia msimu huu wa 2022/23 mpaka 2026/27 kwenye mikataba miwili yenye jumla ya thamani ya Zaidi Tsh Bilioni 10.9.”

“Leo ni mwendelezo wa safari ya mafanikio sio tu kwa GSM na Yanga bali kwa taifa la Tanzania kwa ujumla. GSM ni kampuni ya kizalendo na itaendelea kujikita katika kustawisha mpira wa miguu Pamoja na michezo hapa nchini.”

Tuchel: Nimesikitishwa sana kuondoka Chelsea
Kocha Mtibwa Sugar aitisha Young Africans