Imeelezwa kuwa Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mubiru Abdallah, amesema hafurahishwi na mazingira ndani ya kikosi hicho kutokana na kutotimiziwa mahitaji yake, akitishia ‘kung’atuka’.
Mbeya City ambayo inajivunia rekodi ya kudumu kwenye Ligi Kuu tangu ilipopanda msimu wa 2013/14, imekuwa ni kati ya timu zenye mashabiki wengi kwenye ligi kwa miaka ya hivi karibuni.
Msimu huu ilikuwa na mwanzo mzuri ikitabiriwa makubwa katika kuzipa changamoto Simba SC, Young Africans na Azam FC lakini hali imekuwa kinyume na matarajio ya wengi.
Awali, ilielezwa tatizo linalowakabili wachezaji ni kutopewa bonasi wanazoahidiwa na mabosi hali iliyowafanya wapoteze morali baada ya kucheza takribani 12 na kukosa matokeo mazuri.
Mubiru amesema kwa sasa hafurahii mazingira kwani hata kwenye mapendekezo aliyohitaji hakuna utekelezaji uliofanywa na kila mtu anafanya lake.
Kocha huyo ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha dirisha dogo alipendekeza usajili wa wachezaji saba, lakini hadi sasa ameshangazwa hakuna dalili za utekelezaji huku ishu ya matokeo mabovu akitupiwa lawama yeye.
“Hii siyo akademi kwamba nianze kufundisha. Hao unaowaona wamekuja majaribioni sina taarifa nao, nilipeleka ripoti lakini hakuna kilichofanyika, sasa nifanyeje? Mungu ndiye anajua kama msimu utaisha nikiwa hapa,” amesema kocha Mubiru
Mbeya City Jumanne (Januari 17) itacheza Mchezo wa Mzunguuko wa 20 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mchezo wa Duru la Kwanza uliozikutanisha timu hizo mjini Mbeya, ulimalizika kwa sare ya 1-1, Simba SC ikitangulia kufunga kupitia kwa Kiungo Muzamiru Yassin na baadae Tariq Seif aliisawazishia Mbeya City.