Baada ya kurejea jijini Dar es salaam wakitokea Arusha jana Jumapili (Agosti 21), Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Mohamed Nabi amesema atautumia muda wa majuma mawili kukiongezea makali kikosi chake.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia anatarajia kutumia muda huo, kufuatia Ligi Kuu Tanzania Bara kusimama kupisha michezo ya Kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ ambapo Tanzania itacheza dhidi ya Uganda.
Nabi amesema amedhamiria kuutumia muda huo ili kukamilisha maandalizi ambayo aliyafanya kabla ya kuanza kwa msimu mpya, huku akidai hakuwa na muda mzuri wa kukamilisha alichokipanga kwa wachezaji wake.
Amesema baada ya kurejea jana Jumapili (Agosti 21), Wachezaji wake watapumzika kwa siku mbili na kisha wataanza kambi kuendelea na maandalizi kwa muda wa majuma mawili ambayo amedhamiria kufanya jambo.
“Tulikua na siku chache za maandalizi hivyo ninahitaji kutumia muda wa majuma mawili kubaki na wachezaji wangu ambao hawajaitwa timu ya taifa ili kujenga muunganiko mzuri,”
“Nina wachezaji wengi wazuri na bora, ila bado hawana muunganiko mzuri licha ya kupata matokeo mazuri katika michezo miwili ya awali ya Ligi. Sijaona ninachokihitaji kutoka kutoka kwao, hivyo ninaamini wakipumzika siku mbili na kurudi nitaweza kufanya kilicho bora.” amesema Nabi
Katika hatua nyingine Kocha Nabi amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kuvuana alama sita ugenini katika michezo miwili waliyocheza ugenini Uwanja wa Sheikh Amri Abeid dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union.
Kocha huyo anaamini alama sita walizozivuna ugenini zitasaidia katika mbio zao za kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2022/23.