Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasredine Mohamed Nabi, ametabiri upinzani mzito kutoka kwa Al Hilal ya Sudan, katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mchezo huo wa Mzunguuko wa Kwanza hatua ya Mtoano, umepangwa kupigwa kesho Jumamosi (Oktoba 08) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam saa kumi jioni.
Kocha Nabi amezungumza na Waandishi wa Habari leo Ijumaa (Oktoba 07) Mchana na kueleza mipango na mikakati atakayoitumia kwenye mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu kubwa na Mashabiki wa Young Africans.
“Ni mchezo wa kupata matokeo ya kufuzu tumejiandaa tukiwa tumetulia hatuongei sana tunajua mashabiki wanahitai nini tunafanya kazi bila fujo na kwa kutulia,”
“Tunaenda kukutana na timu nzuri timu yenye historia nzuri kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.”
“Naamini Al Hilal wanaiheshimu Young Africans na ndio maana hata wamecheza michezo mingi ya kirafiki ili kujiandaa dhidi yetu. Matokeo yao dhidi ya TP Mazembe hayatufanyi tubweteke.”
“Tumeandaa Wachezaji vizuri na mchezo huu hautaishia kwa Mkapa. Mchezo itaisha baada ya filimbi ya mwisho itakapopulizwa pale Khartoum, Sudan.”
“Hivyo wachezaji wanatambua hilo na wako tayri kupambana huku wakijua mchezo huu hautaishia kwa Mkapa.” amesema Kocha Nabi
Kuhusu madhaifu yaliyojitokeza kwenye kikosi chake, Kocha Nabi amesema ameyafanyia kazi madhaifu yaliyojitokeza siku za karibuni kwa kuwaandaa wachezaji wake, ili wasirudie makosa ambayo huenda yakawagharimu dhidi ya Al Hilal.
“Tunajua tumefungwa kupitia magoli mawili kwa kona ni sababu ya wachezaji kukosa umakini ila tumewaonesha wachezaji video japo kuwa wao [Al Hilal] wana miili mikubwa tofauti na Young Africans lakini tunajua namna ya kuwakabili, hatuwezi kusema vitu vyote hapa sababu tutakuwa tumewapa ya kujiandaa kutukabili.” amesema
Young Africans ilitinga Mzunguuko wa Kwanza kwa matokeo ya jumla 9-0 dhidi ya Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC, huku Al Hilal ikisonga mbele kwa faida ya bao la ugenini, kufutia ushindi wa jumla wa sare ya 2-2.
Ikicheza ugenini Ethiopia dhidi ya St George mwezi Septemba Al Hilal ilikubali kufungwa 2-1, kabla ya kuibuka na ushindi wa 1-0 mjini Khartom.