Wakati Kikosi cha Simba SC kikiwasili salama mjini Ruangwa mkoani Lindi tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara mzunguuko wa 27 dhidi ya Namungo FC, Kocha Mkuu wa timu mwenyeji ametoa kauli nzito inayothibitisha dhamira ya kuzitaka alama tatu muhimu za mchezo huo.

Miamba hiyo ya Ligi Kuu itakutana kesho Jumatano (Mei 03) katika Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, huku Namungo FC ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wa Duru la kwanza uliopigwa Novemba 16 mwaka jana (2022) kwa bao 1-0, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kocha Mkuu wa Namungo FC Denis Kitambi amesema huu ni wakati sahihi kwao wa kuweza kufuta uteja mbele ya Simba SC ambayo wameshindwa kuifunga tangu walipoanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara misimu mitatu iliyopita.

Kitambi amesema licha ya ugumu wa mchezo huo ila ni muda wa kuondoa unyonge mbele ya wapinzani wao kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri kila wakati wanapokutana.

“Awali malengo yetu yalikuwa ni kumaliza nafasi nne za juu lakini ukiangalia kasi ya washindani wetu na kutokuwa na matokeo mazuri imeturudisha nyuma hivyo angalau tumalize ya tano,” amesema

Kitambi ameongeza katika michezo yote iliyobaki wameanza kampeni ya kuhakikisha kila mpinzani atakayefika uwanjani mwao anakutana na wakati mgumu wa afasi lakini kupata ushindi ili kasi kutimiza malengo ndani yao.

Katika michezo saba ya Ligi Kuu Bara ambayo Namungo imecheza na Simba SC tangu msimu huo imepoteza mitano na kupata sare miwili tu na imefungwa jumla ya mabao 14 huku wao wakifunga matano tu.

Mchezo huu ambao utapigwa Kesho Jumatano (Mei 3) unarudisha kumbukumbu ya mchezo baina ya timu hizi uliopigwa pia Mei 3, mwaka jana (2022) wakati miamba hii ilipokutana kwenye Uwanja wa Ilulu na kufungana mabao 2-2.

Katika mchezo huo mabao ya wenyeji Namungo yalifungwa na Jacob Masawe na Obrey Chirwa huku kwa upande wa Simba SC yakifungwa na beki wa kulia, Shomari Kapombe pamoja na mshambuliaji Kibu Denis.

Kwenye michezo 26 iliyocheza timu hiyo imeshinda 10, sare mitano na kupoteza 11 ikiwa nafasi ya sita na alama 35.

Yondani awashangaa wanaoibeza Simba SC
Ofa zapishana Msimbazi, Robertinho atuliza mzuka