Baada ya kuwasili Mjini Unguja Visiwani Zanzibar, Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC franco Pablo Martin ametamba kutwaa taji la Mapinduzi 2022.
Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema wamekwenda visiwani humo kwa ajili ya kushinda pia kuhakikisha wanarejea Dar es Salaam na Ubingwa wa Michuano hiyo, ambao utakua wa kwanza kwake na klabu hiyo kwa mwaka 2022.
Amesema licha ya uwapo wa wachezaji wake wote, atafanya mabadiliko ya mara kwa mara ya kikosi ili kuwalinda wachezaji kwa sababu wana majukumu makubwa baada ya michuano hiyo.
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunatoa ushindani na kutwaa ubingwa, hatukufanya vizuri kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita na tunataka kubadili upepo na kuwa mabingwa wa michuano hii,” amesema Pablo.
Amesema wanahitaji kufanya vizuri pamoja na kuyatumia mashindano hayo kama mazoezi kwa kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza katika mechi zilizopita ili kujiweka tayari kuelekea michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu itakaporejea.
“Hii michuano ni muhimu sana kwetu, tukiwa na malengo ya kutwaa ubingwa pia kuimarisha kikosi chetu kuelekea katika michuano mingine iliyopo mbele yetu,” amesema kocha huyo.
Ubingwa wa michuano hiyo unashikiliwa na Young Africans , ambayo iliutwaa mwaka jana (2021) kwa kuwafunga watani zao wa jadi, Simba kwenye Uwanja wa Amaan Zanzibar kwa mikwaju ya Penati 4-3, baada ya kutoka suluhu kwa dakika 90 za mchezo.