Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amewajibu baadhi ya wadau wa soka nchini Tanzania wanaohoji, maamuzi yake ya kubadilisha kikosi mara kwa mara.
Simba SC imekua na wakati mgumu wa kutokua na kikosi cha kwanza tangu alipokuja Kocha huyo kutoka nchini Hispania, akichukua nafasi ya Kocha Didier Gomes aliyesitishiwa mkataba wake, baada ya klabu hiyo kung’olewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika mwezi Oktoba mwaka 2021.
Kocha Pablo amesema sababu kubwa inayomfanya kubadilisha kikosi mara kwa mara, imeegemea kwenye suala la kiufundi kutokana na anavyowafuatilia wachezjai wake siku hadi siku.
Amesema asilimia kubwa ya wachezaji wake wameshindwa kuwa kwenye kiwango cha kidumu, na inamuuwia vigumu kuwatumia mara kwa mara kwa kuhofia mambo kumuendea kombo.
“Sina kikosi cha kwanza kwa sababu wachezaji hawana muendelezo mzuri wa ubora wao siwezi nikamtumia mchezaji ambaye ameshindwa kunionyesha kitu kwenye mazoezi eti kwa sababu amefanya vizuri mchezo uliopita.” amesema Kocha Pablo
Pamoja na kufanya maamuzi ya kubadilisha kikosi mara kwa mara, Kocha Pablo ameonyesha kuwaamini baadhi ya wachezaji wa Simba SC kama Mlinda Lango Aishi Manula, Mabeki Mohamed Hussein, Shomari Kapombe. Joash Onyango na Henock Inonga.