Siku tatu kabla ya mpambano wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia chini ya Umri wa miaka 20, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 Tanzanite, Bakari Shime, amesema amekiandaa vyema kikosi chake kushinda mchezo huo.
Tanzanite itachuana na Nigeria Jumapili (Novemba 12) katika mchezo wa Mzunguuko watatu wa kuwania kufuzu Kombe la Dunia, utakaochezwa katika dimba la Azam Complex jijini Dar es Salaam.
Kikosi cha Tanzanite kimetinga raundi hiyo baada ya kuitoa Djibouti kwa mabao 12-0 katika Mzunguuko wa pili.
Kocha Shime amesema anaendelea kukipa mbinu kikosi chake kiweze kushinda mchezo huo.
“Maandalizi yanaendelea vizuri, Watanzania wategemee matokeo mazuri kutoka kwa Tanzanite, pia malengo ya timu ni kufuzu Kombe la Dunia,” amesema Shime.
Kocha huyo aliwaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa hamasa ili Tanzanite ifanye vizuri katika mchezo huo.
“Sapoti ya Watanzania ni muhimu, tunawaomba wajitokeze kwa wingi kuiunga mkono timu yetu, nina imani umoja wao utawapa nguvu wachezaji kufanya vizuri katika mchezo huo,” amesema Shime.