Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesisitiza bado anaendelea kuangalia viwango vya wachezaji wote na kuona jinsi atakavyowatumia, licha ya kukiongoza kikosi hicho kwenye michezo mitatu mfululizo na kushinda.
Kauli ya Sven imekuja kufuatia kuwa na vikosi tofauti tangu akabidhiwe timu hiyo hivi karibuni.
Michezo hiyo ni ule wa Kombe la Shirikisho la Azam (FA) akiwang’oa Arusha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza na kuendeleza moto huo kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara akianza kuvuna ushindi dhidi ya Lipuli FC kwa mabao 4-0 na 2-0 dhidi ya KMC.
Katika michezo hiyo mitatu, kocha huyo pamoja na msaidizi wake, Selemani Matola, bado hawajaruhusu nyavu zao kufungwa bao tangu waliporithi mikoba hiyo kutoka kwa benchi la ufundi lilopita chini ya Mbeligiji Patrick Aussems ambao waliong’olewa kwa kushindwa kusimamia nidhamu ya nyota wa kikosi hicho.
Kocha huyo alisema timu hiyo ina kikosi kipana na tangu amejiunga na mabingwa hao bado hajafanikiwa kuwaangalia wachezaji wote ila ameandaa mfumo utakaomuwezesha kufanikiwa hilo.
“Tangu nimejiunga na timu nimefanikiwa kuiongoza kwenye michezo mitatu ya kimashindano na tumeshinda yote nafikiri ni mwanzo mzuri kwangu ingawa ninachoweza kusema hadi sasa bado sijaangalia uwezo wa wachezaji wote,”amesema.