Kocha Mkuu wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amewaomba radhi Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kufuatia kichapo cha 1-0, walichokipata mbele ya Kagera Sugar.
Simba SC ilipoteza mchezo huo ikiwa ugenini mjini Bukoba mkoani Kagera jana Jumatano (Januari 26), huku bao la ushindi la Kagera Sugar likipachikwa wavuni na Mshambuliaji kutoka nchini Uganda Khamis Kiiza ‘Diego’.
Kocha Pablo amesema imekua bahati mbaya kwa kikosi chake kupoteza mchezo huo, hivyo hana budi kuomba radhi kwa kilichotokea Uwanja wa Kaitaba.
“Ni matokeo ya kusitikisha sana, hatukutarajia kwa sababu tulijiandaa kushinda, imeniuma sana kupoteza alama tatu hapa, niwateke radhi Mashabiki ambao walikua na matumaini na timu yao leo (Jana).” Amesema Pablo.
Simba SC imepoteza mchezo wa pili msimu huu 2021/22, huku ikitoka sare mara nne, hali ambayo inaifanya kumiliki alama 25 zinazoiweka nafasi ya pili kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Young Africans inaongoza Msimamo ikiwa na alama 35, huku ikicheza michezo 13 sawa na Simba SC.