Kocha wa viungo wa Simba SC, Mnyarwanda, Corneille Hategekimana amefichua siri kuwa anashangazwa na uwezo mkubwa wa wachezaji wa timu hiyo kuelewa haraka mbinu za mazoezi anayowapa, huku akitoa onyo kali kwa wapinzani wao wakiwamo Young Africans kwenye Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mtaalam huyo ametoa kauli hiyo baada ya kuanza kazi rasmi ndani ya kikosi hicho kilichoweka kambi nchini Uturuki kwa ajili ya kujianda na msimu ujao wa ligi na michuano ya kimataifa.
Hategekimana amesema kuwa, wamepata sehemu nzuri yenye ubora mkubwa wa kufanya maandalizi na tangu wamefika nchini humo ni siku nne ambazo wamefanya mazoezi huku wachezaji wakionekana kuelewa kwa haraka tofauti na matarajio yake.
Amesema licha ya kutokamilika kwa wachezaji wote ndani ya kikosi anaimani kubwa mwisho wa Pre Season watakuwa vizuri zaidi kuanzia utimamu wa mwili, kiufundi na mbinu za uwanjani.
“Tangu tumefika hapa tulifanya mazoezi ya viungo Gym, tukaenda kwenye bwawa la kuogelea ambalo kuna mazoezi yake ni muhimu na kumjenga mchezaji utimamu wa mwili na tumekuwa na programu ya uwanjani kwa kocha Robertinho kuanza kufanya majukumu ya mbinu za kiufundi.
“Tuna timu nzuri wachezaji wameonyesha kuelewana kwa kile kinachotolewa kutoka kwetu wanajua nini wanatakiwa kufanya wanapokuwa na mpira au hawana mpira jinsi ya kujilinda na mpinzani, huko mbele kutakuwa na kazi kubwa kwa wapinzani,” amesema Hategekimana.