Kocha Mkuu, Sven Vandenbroeck amefurahishwa na viwango vya wachezaji wanavyoonyesha wakiwa mazoezini hali inayompa matumaini ya kufanya vizuri kwenye michuano ya ligi Kuu na Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC).
Sven amesema wachezaji wanaonyesha morali ya hali ya juu na kujitahidi kufuata maelekezo huku kila mmoja akihitaji kupewa nafasi ya kuaminiwa kitu ambacho kitampa wigo mpana wa kupanga timu ligi ikirejea mwishoni mwa juma.
Sven ameongeza kuwa katika siku nne zilizobaki kabla ya kukutana na Ruvu Shooting katika mchezo wa kwanza wa ligi, akiwa mazoezini atasisitiza katika mbinu zaidi kwa wachezaji pamoja na stamina.
“Nimeridhishwa na viwango vya wachezaji wangu mazoezini, morali iko juu na wanajitahidi kufuata maelekezo tunayowapa. Kabla ya mechi yetu ya kwanza tutahakikisha tunajifunza zaidi mbinu za mchezo,” amesema Sven.
Kuhusu mechi mbili za kirafiki zilizochezwa juzi kwenye uwanja wetu wa Mo Simba Arena, Kocha Sven amesema hakuangalia zaidi matokeo badala yake ameangalia jinsi wachezaji walivyofanikiwa kutimiza majukumu yao vizuri.
“Kwenye mechi za kirafiki binafsi nimeangalia zaidi jinsi wachezaji walivyocheza, walivyotimiza majukumu uwanjani matokeo ilikuwa ni jambo la pili ambalo nalo limenifurahisha,” amesema kocha Sven.
Akizungumza kuhusu hali ya kiungo Jonas Mkude, Kocha Sven amesema hajui mpaka sasa atamkosa nyota huyo kwa muda gani kwa kuwa anasubiri vipimo zaidi kutoka kwa daktari ili kujua ukubwa wa jeraha.