Ushindi wa 2-3 dhidi ya Namungo FC umempa jeuri Kocha Mkuu wa Maafande wa Jeshi la Magereza ‘Tanzania Prisons’ Mohamed Abdallah ‘Bares’, ambaye ana jukumu la kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja mwishoni mwa msimu huu.
Tanzania Prisons juzi Jumamosi (Machi 11) ilichomoza na ushindi huo ugenini katika Uwanja wa Majaliwa mjini Ruangwa-Lindi, ambao umeifanya timu hiyo kufufua matumaini ya kuendelea kupambana kwa lengo la kubaki Ligi Kuu.
Kocha Bares amewataka mashabiki Tanzania Prisons wawe na Imani, kwani timu yao ipo katika mikono salama na haitashuka Daraja licha ya Presha ambayo wanaipitia pamoja na mwendo ambao hawaufurahii.
“Unaona timu inacheza na wachezaji wana presha kubwa ya kupata matokeo mazuri hilo linawafanya wapambane na wanaonyesha uwezo mkubwa hivyo bado tuna nafasi ya kubaki kwenye ligi.”
“Ninachoweza kuwaambia mashabiki ni kwamba wawe na imani, tunaamini tutabaki kwenye ligi kwani mechi zipo na pointi 25 ambazo tunazo sio haba muhimu ni kupambana kwani huu ni mpira na kila kitu kinawezekana.” Amesema Bares
Tanzania Prisons haikuwa kwenye mwendo mzuri katika michezo yake ya hivi karibuni, Februari 25 ilishuhudia ubao wa Uwanja wa Mkwakwani ukisoma Coastal Union 1-0 Prisons mchezo wa ligi na iliondolewa hatua ya 16 bora na Young Africans Machi 03, 2023 Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kufungwa mabao 4-1 Uwanja wa Azam Complex.
Kwenye msimamo Ligi Kuu Tanzania Bara, Prisons ipo nafasi ya 13 ikiwa imecheza michezo 25 ikiwa na wastani wa kukusanya alama moja kwenye kila mchezo.